The Character of Holy Ghost (Tabia na Kazi za Roho Mtakatifu)

Share it Please

 


                                  Askofu Zachary Kakobe 

 

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   TABIA NA KAZI ZA ROHO MTAKATIFU

Siku ya leo ya Kuichambua Biblia, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tutatafakari kwa makini YOHANA 16:5-22.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tunajifunza, “TABIA NA KAZI ZA ROHO MTAKATIFU“.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vinne:-











(1)      YESU MWALIMU WA MFANO (MST. 5);

(2)      TABIA NA KAZI ZA ROHO MTAKATIFU (MST. 8-11, 13-15);

(3)      HEKIMA YA KUWALEA WATOTO WACHANGA KIROHO (MST. 12);

(4)      HUZUNI KUGEUKA KUWA FURAHA (MST. 6-7, 16-22).

 

(1)         YESU MWALIMU WA MFANO (MST. 5)

Yesu Kristo, Mwalimu wetu, katika mstari huu, anawauliza wanafunzi wake, “Wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwenda wapi?“.  Siyo kwamba wanafunzi wake walikuwa hawajauliza kabisa swali hili.  Petro aliuliza swali hili katika YOHANA 13:36, na Tomaso aliuliza swali lililokuwa na maana hiyo katika YOHANA 14:5.  Hata hivyo, baada ya wanafunzi hawa kuuliza swali hili mara mbili, hawakumwuliza tena.  Yesu alitaka wazidi kumwuliza, maana aliwaona bado hawajaelewa.  Hapa, Yesu anatoa mfano kwa Walimu wote wa biblia.  Furaha ya Mwalimu yeyote wa Biblia anayefuata mfano wa Yesu, ni kuona wanafunzi wake wanaelewa, na kuyatendea kazi yale wanayofundishwa.  Mwalimu wa Biblia, hataridhika kuona anafundisha tu wakati wanafunzi wake hawamwelewi.  Furaha yake itakuwa kuona wanafunzi wake wanauliza maswali tena na tena ili wapewe ufafanuzi kwa njia iliyo rahisi zaidi mapaka waelewe.  Mwalimu wa Biblia anayefuata mfano wa Yesu, hatachoshwa na maswali au kuyachukia, ikiwa wanafunzi hao watakuwa wanauliza maswali hayo kwa lengo la kutafuta kuelewa.  Sisi nasi kama wanafunzi wa Yesu, tunakumbushwa kuwa na bidii kuuliza maswali tena na tena, mpaka tuelewe, na kuishindania imani.  Wanafunzi wengi wa yesu, huona aibu kuuliza maswali na kuogopa kuonekana kuwa hawajui.  Kufanya hivyo kunatuweka katika hatari ya kuiacha imani kutokana na kutokuelewa, na kupata hasara ya milele.  Petro alikuwa mwulizaji mkubwa wa maswali.  Kutokana na maswali yake, tunapata mafundisho mengi ambayo tusingeyapata.  Kwa mfano, Petro bila aibu, anamwuliza Yesu katika MATHAYO 18:21  “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nimsamehe? Hata mara saba?“  Kutokana na swali hili, wote tunapata mafundisho kuhusu kusamehe.

 

(2)         TABIA NA KAZI ZA ROHO MTAKATIFU (MST. 8-11, 13-15)

Katika mistari hii, tunajifunza kuhusu tabia na kazi za Roho Mtakatifu.  Ingawa Roho Mtakatifu ana tabia na kazi nyingi zaidi kuliko zile zilizoorodheshwa hapa, hata hivyo, katika mistari hii, tunajifunza tabia na kazi zake za msingi.  Zifuatazo ni kazi za Roho Mtakatifu zinazotajwa katika mistari hii:-

 

  1. KUUHAKIKISHIA ULIMWENGU KWA HABARI YA DHAMBI: – Watu wote ambao hawamwamini Yesu, wanafanya dhambi (MST. 9).  Watu wengi ingawa hawamwamini Yesu, hujihesabia haki kutokana na amtendo yao kama Farisayo yule katika LUKA 18:9-14.  Watu wengi hujihesabia haki na kujiona kwamba hawana dhambi, kwa kuwa wanashika taratibu zote za dini zao, kama walivyofundishwa (MATENDO 26:4-5; WAGALATIA 1:14).  Kutokana na msingi huu, Sauli alijihesabia haki na kuona kwamba yeyote ambaye alikuwa hafuati taratibu zote za dini yake, ndiye mwenye dhambi na alifaa hata kuuawa.  Aliposikia sauti ya Yesu ikisema, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi?  Alishangaa, maana aliona anatenda haki yote.  Tukitoka na kwenda kuwahubiria watu wa jinsi hii ya Farisayo na Sauli, na kutaka waokolewe, bila msaada wa Roho Mtakatifu, hatuwezi kufanikiwa, kwa sababu wao watajiona kuwa hawana dhambi na kutuona sisi ndiyo tuliopotea kwa sababu hatuko katika dini zao!  Mtu ambaye havuti sigara, hanywi pombe, haibi, hafanyi ushirikina, haui au hatukani matusi, mtu wa namna hii ni vigumu kumshawishi kwamba ana dhambi, na kumtaka atubu na kuokolewa, kwa kumfundisha tu kwamba, sisi sote tumefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu tangu kuzaliwa (ZABURI 51:5; WARUMI 3:10-12, 23; 1 YOHANA 1:8-10).  Sasa basi, ni kazi ya Roho Mtakatifu kumfanya kila mtu wa namna hii, anayejihesabia haki, kushtakiwa na dhamiri yake na kujiona hafai na ni mwenye dhambi (YOHANA 8:3-9).  Ndiyo maana, tukitoka kuwahubiri watu na kutegemea ujuzi wetu tu wa maandiko bila msaada wa Roho Mtakatifu, hatuwezi kupata matokeo makubwa.  Hatuna budi wakati wote kuitambua kazi hii ya roho Mtakatifu, na kumkaribisha aambatane pamoja nasi kila tunaposimama kuhubiri au kufundisha ili ashuhudie pamoja nasi (YOHANA 15:26-27).  Tukifanya hivi, huduma zetu zitakuwa na mafanikio makubwa.  Hatuna budi kupokea uwezo utokao juu, Nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuwe mashahidi wa Yesu wenye uwezo wa kuwaleta wenye dhambi wengi kwa Yesu (LUKA 24:48-49; MATENDO 1:4,8).

 

  1. KUUHAKIKISHIA ULIMWENGU KWA HABARI YA HAKI: – Ni kazi ya Roho Mtakatifu kumhakikishia kila tunayemhubiri kwamba Yesu Kristo pekee ndiye mwenye haki na tunahesabiwa haki kwa kumwamini Yeye tu (1 YOHANA 2:1).  Roho Mtakatifu akitenda kazi hii humfanya mtu akiri kwamba Yesu ndiye mwenye haki, kama ilivyokuwa kwa akida katika LUKA 23:47.  Vivyo hivyo, Roho Mtakatifu huwahakikishia watu tunaowahubiria kwamba maneno yale tunayoyasema ndiyo ya haki, na kweli., kuliko yale waliyojifunza katika dini zao.  Tukiwa na Roho Mtakatifu, hatuna haja ya kutumia Misahafu ya dini nyingine kuwahakikishia watu tunavyowahubiri.  Kufanya hivyo, ni ubatili, maana ni kuvithibitisha vitabu hivyo kwamba vina ukweli, na hilo haliwezi kuleta matokeo.
  1. KUUHAKIKISHIA ULIMWENGU KWA HABARI YA HUKUMU: – Watu wengi wenye dhambi, hawaamini kwamba kuna hukumu ya kutupwa motoni baada ya kufa, na kuona kama ni mbinu za kuwaanya waache starehe za dunia.  Watu wengi pia hawaamini kwamba wanaweza kusamehewa dhambi zao kabisa na kufutiwa hukumu, na hudhani kwamba hata wafanyeje kama wameandikiwa motoni basi.  Kazi ya roho Mtakatifu, ni kumhakikishia mtu tunayemhubiria kwamba ni kweli kuna hukumu baada ya kufa na Mhukumu wa Ulimwengu huu ni Yesu.  Vilevile humhakikishia kwamba Mkuu wa Ulimwengu Shetani, yeye amekwisha kuhukumiwa kutupwa katika moto wa milele, na hana nafasi ya kusamehewa, laki8ni sisi tuna nafasi ya kufutiwa hukumu tukimwamini Yesu (WAEBRANIA 9:27; MATHAYO 25:41; YOHANA 3:18, 36).  Kwa msaada wa Roho Mtakatifu ndipo mtu anapoweza kusema kama mhalifu msalabani katika LUKA 23:39-42.

 

  1. KUWAONGOZA WATU NA KUWATIA KWENYE KWELI YOTE: – Roho Mtakatifu, huwaongoza watu na kuwaonyesha njia ya kweli.  Anaweza hata kusema na watu kwa njia ya ndoto kama mkewe Pilato (MATHAYO 27:19), na kuwaelekeza waende kusali Kanisa fulani, waende katika mkutano fulani wa Injili n.k.  Roho Mtakatifu huwapeleka watu kwenye kweli.  Ndiyo maana tukiwa hatuhubiri kweli katika makanisa yetu, tutaona watu wengi wanachomoka na kuhama wakiongozwa na Roho Mtakatifu kwenye kweli yote, na kwa kukosa ufahamu, tutalalamika kwemba watu wetu WANAIBIWA!  Roho Mtakatifu hawaibi!  Ni watu wake!  Roho Mtakatifu huwaongoza watu kwa wingu na moto (HESABU 9:15-23).  Tabia za Roho Mtakatifu, ni pamoja na hizi zifuatazo tunazojifunza katika mistari hii:
  1. HANENI KWA SHAURI LAKE MWENYEWE: – Maneno ya Roho Mtakatifu SIKU ZOTE hufanana na maneno ya Yesu, hayatofautiani kamwe maana Roho Mtakatifu hutwaa katika yaliyo ya Yesu na kutupasha habari (MST. 13-15).  Yeye ni roho wa kweli, na Yesu ndiye Kweli, hivyo ni sawa pia kusema Yeye ni Roho wa Yesu (MATENDO 16:7).  Roho Mtakatifu, hushuhudia pamoja na Baba na Mwana (1 YOHANA 5:8).  Hivyo mtu akisema ameongozwa na Roho Mtakatifu kumwacha mkewe na kumwoa mke mwingine, ni dhahiri kwamba huyo siyo Roho Mtakatifu, maana Yesu alisema amwachaye mkewe na kumwo mwingine azini, na Baba anachukia kuachana (LUKA 16:18; MALAKI 2:15-16).  Ujumbe au unabii wowote unaodaiwa kwamba unatokana na Roho Mtakatifu, kwa msingi huu, lazima tuupime kwa Neno la Mungu.
  2. NI ROHO WA KWELI: – Hasemi uongo, hivyo ujumbe unaotokana na Roho Mtakatifu unaotupasha habari ya mambo yajayo, hauna budi kutimia.  Hata hivyo, hata ukitimia, lakini unatutoa mbali na kweli ya Neno la Mungu, tujue pia siyo wa Roho Mtakatifu (KUMBUKUMBU 13:1-4).  Inatupasa kuwa waangalifu nyakati za leo kuweka mawazo yetu katika unabii, Roho hutumia njia hii leo mara chache sana, maana anasema nasi leo katika Neno la Mwana wa Mungu Yesu (WAEBRANIA 1:1-2).  Katika Matendo ya Mitume,

tunaona jumbe chache sana za Roho Mtakatifu kwa miaka mingi!

(3)         HEKIMA YA KUWALEA WATOTO WACHANGA KIROHO (MST. 12)

Hata kama tunafahamu mafundisho mengi, hatuna budi kuwafundisha watoto wachanga kiroho hatua kwa hatua, tukiwapa maziwa kwanza.  Tukianza tu kuwafundisha mafundisho magumu mwanzoni, hawawezi kuyastahimili.  Hatuna budi kuwaongoza polepole, tukiwaharakisha watakufa kiroho (MWANZO 33:12-14; 1 PETRO 2:2).

 

(4)         HUZUNI KUGEUKA KUWA FURAHA (MST. 6-7, 16-22)

Matatizo na dhiki tulizo nazo duniani leo, zinafananishwa na uchungu wa uzazi hasa ule wa mtoto wa kwanza (YEREMIA 4:31; 6:24).  Wanafusnzi wa Yesu waliona huzuni Yesu kuwaacha kumbe ilikuwa furaha kwao maana ndipo Roho Mtakatifu anagekuja kwao.  Alipokuja Roho kwao, walifurahi na kusahau huzuni yao (MATENDO 13:52).  Leo tunaweza kuwa na huzuni wakati wa ugonjwa utakaotuuua, lakini tukifa, tutasahu uchungu wote, ikiwa tutakufa tukiwa tumeokoka.  Mateso na dhihaka za waume, wazazi, kukosa hiki au kile kwa ajili ya wokovu, yote haya ni utungu ambao utatuletea furaha kama ya kujifungua mtoto, tutakapomwona Yesu.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

No comments:

Post a Comment