Bwana Yesu asifiwe sana wana wa Mungu, ni matumaini yangu na Imani yangu ya kwamba u mzima na ya kuwa unaendelea kuufurahia uzuri wa Yesu Kristo na kazi yake ya msalaba.
Leo ninataka kwa pamoja tuyachunguze maandiko na tuzipitie sababu hizi saba za Kibiblia ni kwa nini watu wengi wanakufa mapema…na sasa ongezeko la vifo vya mapema ni kubwa kuliko hata zamani. Kwa Tanzania wastani wa kiwango cha maisha ni miaka 45,Binafsi nauona umri huu kuwa ni mdogo sana kwa mtu wa rika hili kuondoka duniani kwani anakuwa na majukumu mengi ya kufanya na pia mchango wake unakuwa unahitajika kwenye familia, ukoo, wilaya, mkoa, taifa na hata duniani kwa ujumla.
Ni maombi yangu na dua yangu kwa Bwana ya kwamba umalizapo kusoma ujumbe huu, macho yako ya ndani yatafunguka na utaweza kuona swala hili kwa jicho la Rohoni…KARIBU SANA.
Zifuatazo ni sababu saba kwa mujibu wa Neno la Mungu ni kwanini watu wanakufa mapema(katika umri mdogo)
1.KUTOWAHESHIMU WAZAZI(BABA NA MAMA)
Biblia iko wazi sana na imesisitiza uhusiano mzuri na wa uhakika kati yetu na wazazi wetu…kinyume chake LAANA zitayaandama maisha yetu na maisha yetu hayatakuwa ya heri na marefu.
Ukisoma Waefeso 6:1-3 inasema, “Enyi watoto watiini WAZAZI wenu katika BWANA, maana hii ndiyo HAKI.Waheshimu baba na mama yako, amri hii ndiyo ya kwanza YENYE AHADI (za ustawi, baraka na wingi wa miaka), upate HERI, UKAE SIKU NYINGI( UISHI SIKU NYINGI) katika dunia” pia katika Kumbukumbu la Torati 5:16 Biblia inasema, “Waheshimu BABA na MAMA yako; kama BWANA, Mungu wako alivyoamuru, SIKU ZAKO ZIPATE KUZIDI, nawe upate KUFANIKIWA katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako”
Kwa mujibu wa maneno ya Mungu hapo juu ni dhahiri kabisa ya kuwa watu wote wasiowaheshimu wazazi wao, ni ngumu kufanikiwa, Laana zinawafuatilia na zaidi ya yote wana muda mchache wa kuishi…WANAKUFA MAPEMA!
2.KUKOSA MAONO
Kwa mujibu wa Biblia, mtu anayeishi ili mradi tu, asiyejua kwanini yupo duniani, asiyekuwa na kusudi na mpango katika maisha yake, na asiyeweza kupanga hata mipango ya ‘kesho nitafanya a, b, c nk’ yuko katika hatari kubwa ya kuondoka duniani kabla ya muda wake…Biblia inasema, “Pasipo MAONO watu huangamia”….Biblia ya kiingereza inasema, “Without VISION people PERISH”
Jitahidi kuwa na maono ya muda mfupi na ya muda mrefu, Mungu anashughulika na walio nacho, wasiokuwa nacho hata kile kidogo walichonacho hunyang’anywa.
3.KUTOKUMCHA MUNGU
Kumcha Mungu ni kuishi maisha yanayoongozwa na HOFU ya MUNGU (si woga dhidi ya Mungu)…Ni maisha ambayo moyo,mwili, nafsi na roho ya mtu inakuwa imejawa na kiu na njaa ya kumpendeza Mungu na kuyafanya maagizo yake yote-tena kwa furaha.
Mithali 10:27 inasema, “KUMCHA BWANA kwaongeza siku za mtu, Bali miaka yao WASIO HAKI itapunguzwa” na pia Mhubiri 7:17 inasema, “Usiwe MWOVU kupita kiasi; wala usiwe mpumbavu; kwanini UFE KABLA YA WAKATI WAKO?”
Kwa mujibu wa ushahidi huu wa Neno la Mungu, ni dhahiri kuwa maisha yasiyo na uchaji na yasiyoongozwa na hofu ya Mungu, yanawafanya wengi wafe kabla ya muda wao waliokusudiwa kuishi.
4.KUMWEKEA MUNGU MIPAKA
Hii ni hali ya mwanadamu kuamini kuwa Mungu anaweza hili na hili hawezi…kitendo hiki Mungu anakiita kuwa ni ‘DHARAU’ kwake… Zaburi 78:41 inasema, “Wakarudi nyuma wakamjaribu MUNGU; Wakamwekea MPAKA Mtakatifu wa Israel”
Mstari huu wa Zaburi unaelezea maisha ya wana wa Israel njiani toka Misri kwenda nchi ya Maziwa na Asali-Kanaani.
Biblia inaeleza jinsi Musa alivyowatuma wapelelezi 12 kwenda kuipeleleza nchi ya ahadi waone kama kama kweli ni nchi ya ‘Maziwa na Asali’…10 kati yao Waliporudi walirudisha ripoti ya kuwa kweli ile nchi ni ya maziwa na asali, ila inakaliwa na Wanefili-wana wa Anaki…majitu na ya kwamba wao ni kama panzi tu na hawawezi kwenda na kuimiliki. Joshua na Kalebu walileta habari njema…waliona kwa macho lakini wakazungumza kile ambacho ni ‘UHAKIKA WA MAMBO YATARAJIWAYO’ wakamwamini Mungu kuwa aweza kuwapa ile nchi kuwa milki yao sawa na alivyomwapia Ibrahim(Hesabu sura ya 13 na ya 14) na wote waliomwekea Mungu mpaka walikufa huko jangwani, hawakuingia nchi ya ahadi…WALIFUPISHA MAISHA YAO KWA KUTOKUAMINI KWAO…Ila Kalebu aliishi muda mrefu sana, alikuwa na nguvu kama za mtu wa miaka 40 hata alipokuwa na miaka 85( soma Joshua 14:6-14) na inaeleza pia ya kuwa Joshua alikuwa MZEE SANA, alikufa akiwa na miaka 110 lakini alikuwa na nguvu zake kamili mpaka pale BWANA alipompumzisha(Joshua24:1-29)
Kama unataka kuwa na maisha marefu, na unataka kuziongeza siku zako…ishi maisha ya IMANI…Usimwekee Mungu mipaka, kumbuka, “Njia zake zi juu mno na fahamu zake pia” Isaya 55:8-11
5.KUTOKUMTUMIKIA MUNGU
Biblia inasema katika KUTOKA 23:25-26, ” Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; NAMI nitakuondolea Ugonjwa kati yako…na hesabu ya SIKU zako nitaitimiza”
Huu ni ukweli ambao inabidi uufahamu na uweke kwenye matendo.Unataka kuishi muda mrefu hapa duniani? kazi ni rahisi…fanya sehemu yako, MTUMIKIE BWANA naye ATAITIMIZA hesabu ya siku zako…HAUTAKUFA KABLA YA WAKATI.
6.MAISHA YA DHAMBI
Dhambi ni mbaya…inakutenga mbali na Mungu( Isaya 59:1-2) lakini kibaya zaidi inapunguza maisha yako…inakufanya ufe kabla ya muda wako…Unafurahia kuishi maisha ya dhambi? ni mzinzi, mwongo, msengenyaji, usiyesamehe,mwenye kinyongo, kisasi nk? Unajipeleka kaburini kabla ya wakati wako…unafanya kazi ambayo mshahara uitwao ‘MAUTI’ utaupata.
Katika Warumi 6:23 Biblia inasema, “Kwa maana mshahara wa DHAMBI ni MAUTI(KIFO), bali karama ya Mungu ni uzima wa Milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” pia Biblia inasema, “Roho itendayo DHAMBI ndiyo itakayokufa”
Maisha ya dhambi yanakata muda wa mtu wa kuishi…Ni wangapi waliokufa wakiwa vijana wadogo kwa sababu ya UKIMWI kwa kutoikwepa dhambi ya Uzinzi? au ni Wezi wangapi wamekufa wakiwa katika harakati za kuiba?
Dhambi ni adui mkubwa kwangu na kwako!
7.KUKOSA BIDII KATIKA KUMPENDA MUNGU
Biblia iko wazi katika Zaburi ya 91:14-16, nayo inasema, “Kwakuwa AMEKAZA(Ameweka bidii katika) KUNIPENDA, Nitamwokoa; na kumweka palipo juu (NITAMWINUA) kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni. Nitamwokoa na kumtukuza; KWA SIKU NYINGI nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu”
Biblia inasema Atakayekaza/kuwa na bidii katika KUMPENDA MUNGU atashibishwa kwa WINGI WA SIKU.
Yesu ameweka wazi ni namna gani waweza kumpenda Yeye, Yohana 14:21 inasema, “Yeye aliye na AMRI zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; Nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”
Nayo Mithali 3:1-2 inasema, ” Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishikeAMRI zangu.Maana zitakuongezea WINGI WA SIKU, NA MIAKA YA UZIMA, NA AMANI“
Unapozishika sheria na Amri alizozitoa Bwana maishani mwako…huo ndo udhihirisho wa Upendo wako kwa Mungu aliye hai…kila unapoongeza bidii ya kumtii na kumheshimu Mungu-ukakaza kumpenda, ANAKUSHIBISHA KWA SIKU NYINGI…Wewe ndiye unayeweza kumwambia Bwana, hii miaka 90 inatosha, nimekwisha shiba maisha…nataka kurudi nyumbani…au miaka 40 inatosha Bwana…nimeshiba siku nataka kurudi nikae na wewe…wewe ndo unayeamua wingi wa siku zako…tangu leo kaza kumpenda BWANA.
Ninaamini umejifunza kitu, na ya kuwa wewe nawe utayagusa maisha ya wengine kwa KWELI hizi ambazo Bwana amesema na wewe kupitia kwangu.Ubarikiwe
Wako katika na Ndani ya Kristo,
Dickson Kabigumila.
No comments:
Post a Comment