Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO: KUFUNGA NI NINI?
(MATHAYO 17:14-21)
Katika MATHAYO 17:14-21, tunajifunza juu ya nguvu ya kufunga. Yako mambo ambayo hayawezekani kama kuomba hakuoanishwi na kufunga. Ni kwa sababu hii basi, tunachukua uzito mkubwa kujifunza kwa undani kuhusu kufunga katika mfululizo wa masomo yanayohusu jambo hili kuanzia leo. Tutaliangalia somo la leo katika vipengele vinne:-
(1) MAANA YA KUFUNGA;
(2) UMUHIMU WA KUFUNGA;
(3) MIFANO YA WATAKATIFU WALIOKUWA WANAFUNGA;
(4) JINSI KUFUNGA KUNAVYOBADILISHA MAMBO.
(1) MAANA YA KUFUNGA
Neno “KUFUNGA“ linatokana na neno la Kiyunani “NESTEVO“, ambalo nalo linatokana na maneno mawili ya Kiyunani “NE“ na “ESTHIO“. Neno “NE“ maana yake “BILA“ au “HAPANA“, Kiingereza “NO“ au “WITHOUT“. Neno “ESTHIO“ maana yake “KULA CHAKULA AU KINYWAJI“, Kiingereza “TO EAT SOLID OR LIQUID FOOD“. Neno “NESTEVO” sasa linaunga maneno hayo mawili ya Kiyunani ”NE” na “ESTHIO”, na lina maana “BILA KULA CHAKULA AU KINYWAJI CHOCHOTE”. Hivyo maana ya kufunga, ni “BILA KULA CHAKULA AU KINYWAJI CHOCHOTE”.
Kufunga siyo kuacha kusoma gazeti ulilozoea, kuacha kuchana nywele n.k., ni kuacha kabisa kula au kunywa kinywaji chochote. Maana hii ya kufunga, inathibitishwa na maandiko yafuatayo:- EZRA 10:6; YONA 3:7; 2 SAMWELI 3:35; ESTA 4:16; KUMBUKUMBU LA TORATI 9:9; MATENDO 9:9.
Kufunga siyo kuacha kula vyakula kama ugali au wali halafu ukawa unakunywa soda, maziwa, uji au kula matunda n.k. Ni kuacha kula chochote wala kunywa chochote kile. Andiko linalotumika kuhalalisha kula vitu vidogo vidogo ni DANIELI 10:2-3. Katika andiko hili “SIKULA CHAKULA KITAMU”, chakula kitamu ni “DESSERTS” kwa Kiingereza au “PUDDING” – ndizi, nanasi, papai, machungwa n.k. Katika mistari hiyo Danieli anasema hakula lolote kabisa.
(2) UMUHIMU WA KUFUNGA (MATHAYO 6:16-18)
Yesu Kristo anamtazamia kila mtu aliyeokoka kuwa na maisha ya kufunga pale anapotuambia “TENA MFUNGAPO“, “BALI WEWE UFUNGAPO“. Kwa jinsi hiyohiyo Yesu anamtazamia kila mtu aliyeokoka kuwa na maisha ya kuomba pale anapotuambia, “TENA MSALIPO“, “BALI WEWE USALIPO (UOMBAPO)“ – MATHAYO 6:5-6. Katika mistari hii tunajifunza kwamba Mungu HUWAJAZI wale wafungao, maana yake HUWAPA THAWABU AU ZAWADI au HUWAJAZA PALE WALIPOPUNGUA.
(3) MIFANO YA WATAKATIFU WALIOKUWA WANAFUNGA
1. YESU KRISTO – Yesu Kristo baada ya kujaa Roho Mtakatifu, alifunga siku arobaini na baada ya mfungo huo alirudi kwa “NGUVU ZA ROHO“ (LUKA 4:1,14);
2. MUSA – (KUTOKA 34:28);
3. EZRA – (EZRA 10:6);
4. ELIYA – (1 WAFALME 19:8);
5. DAUDI – (ZABURI 109:24);
6. PAULO – (MATENDO 9:8-9; 2 WAKORINTHO 11:27);
7. PAULO NA BARNABA (MATENDO YA MITUME 14:23);
8. KANISA LA KWANZA (MATENDO YA MITUME 13:1-3).
Ikiwa watakatifu wengi walifunga katika maisha yao, sisi nasi hatuwezi kupuuza kufunga na tukadai kuwa ni wakristo wa Biblia, vile vile kupuuza kufunga, kutasababisha tuwe dhaifu tukilinganishwa na watakatifu wa zamani.
(4) JINSI KUFUNGA KUNAVYOBADILISHA MAMBO
Sehemu nyingi sana katika Biblia, tunaona jinsi ambavyo mambo yalivyobadilika baada ya kufunga na kuomba. Angalia mifano mitano ifuatayo:-
1. Wana wa Israeli walipigwa mfululizo katika vita na wana wa Benyamini. Baada ya kushindwa mfululizo, wakaamua kufunga na kuomba (WAAMUZI 20:20-22, 24-26). Baada ya kufunga na kuomba matokeo yakabadilika, Benyamini wakapigwa sana, na wana wa Israeli wakashinda vita (WAAMUZI 20:34-35, 41-45, 48). Tunaweza kuitia moto miji yote ya Shetani tukiwa wafungaji, na siyo kinyume cha hapo;
2. Ezra hakumtegemea mfalme, bali alifunga, na matokeo ya kufunga yakawa kwamba mkono wa Mungu ulikuwa pamoja naye na yeye na wenzake wakaokolewa na mkono wa adui (EZRA 8:21-28, 31-33). Ikiwa Kanisa linahitaji kuokolewa kutoka katika mkono wa adui, ni lazima liwe na wafungaji.
3. Yehoshafati alipata taarifa za majeshi kombaini ya Maadui waliotaka kumpiga. Akatangaza kufunga na kuomba (2 MAMBO YA NYAKATI 20:1-4), matokeo yake wakashinda vita kirahisi mno kwa sifa tu (2 MAMBO YA NYAKATI 20:22-25).
4. Nehemia alivyopata taarifa za kubomolewa kwa ukuta wa Yerusalemu na malango yaliyoteketezwa kwa moto, alifunga na kuomba (NEHEMIA 1:3-4), na matokeo yake ukuta ulijengwa tena (NEHEMIA 6:15-16).
5. Hasira ya Bwana kwa Kanisa, Taifa, kutokana na uovu wa watu, inaweza kufanywa kuwa AMANI kwa KUFUNGA NA KUOMBA (1 WAFALME 21:27-29; YONA 3:7-10; EZRA 10:6).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..
No comments:
Post a Comment