Na Askofu Mkuu Silyvester Gamanywa. |
Kizazi chetu cha leo kimegubikwa na changamoto za utitiri wa madhehebu ya Kikristo yenye itikadi zinazokinzana; wakati ambapo yote yanajitambulisha kwa mwavuli mmoja wa Ukristo. Hali hii imesababisha hata ile maana halisi ya Ukristo kupoteza mwelekeo kwa jamii ya wasioamini na ambao wanashindwa kutofautisha ni madhehebu gani yako sahihi na yapi si sahihi.
Hata ukifuatilia kwenye mijadala mbali mbali katika mitandao yetu ya kijamii; utashangaa kuona malumbano ya itikadi za kimadhehebu kujitangaza kuwa mapokeo yake ndiyo sahihi kuliko madhehebu mengine yote. Ukweli ni kwamba haiwezekani itikadi zote zinazokinzana kiitikadi zote zikawa ni sahihi kibiblia. Lazima kuna “Michepuko ya kiimani” ndani ya madhehebu yetu hata kama ni vigumu kukiri au kuipambanua.
Hii ni mada yangu ya kumaliza mwaka 2016. Nia yangu ni kutoa mchango wa kusaidia kupunguza utata uliopo kwa kuanisha vigezo vya kibiblia vya kufanyia tathmini kuhusu usahihi wa imani yetu kwa mujibu wa Biblia. Nitaanzia mbali kidogo lakini ukifuatana nami tutaelewana kwenye hitimisho la mada yenyewe. Karibu:
AINA KUU MBILI ZA UZAO WA BINADAMU WA KIROHO DUNIANI
Tangu binadamu wa kwanza kuasi na kupoteza utukufu wa Mungu; tunasoma tamko la kinabii kutoka kwa Mungu alipokuwa akitoa hukumu ya adhabu kwa nyoka aliyetumika kuambukiza roho ya uasi: “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (MW.3:15)
Maneno haya ni tamko la Mungu dhidi ya nyoka lenye kutaja habari za “uadui” kati ya Nyoka na Binadamu; na “uadui” kati ya “uzao wa nyoka” na “uzao wa mwanamke”! Na hapa ndipo tunapata chimbuko la aina kuu mbili za uzao wa binadamu wa kiroho duniani. Mungu mwenyewe ndiye aliyetaja hii misamiati ya “uzao wa nyoka” na “uzao wa mwanamke.”!
Kwanini natumia usemi wa “uzao wa binadamu wa kiroho”? Ni kwa sababu kuna dhana KONGWE NA potofu inayofundisha kwamba nyoka alifanya tendo la ngono na Eva na akapata ujauzito akamzaa Kaini aliyekuja kumuua ndugu yake na akalaaniwa na Mungu. Dhana hii inabeba tafsiri kwamba dhambi iliyofanyika katika bustani ya Edeni haikuwa kula tunda halisi la mti wa ujuzi wa mema na mabaya na badala yake lilikuwa ni tendo la ngono.
Ukweli wa kibiblia ni kwamba, hakuna ushahidi wala dalili za uwepo wa tendo la ngono kuwa ndiyo dhambi iliyofanyika katika bustani ya Edeni. Mungu aliposema “uzao wa nyoka” kile alichomaanisha ni ile “roho ya kuasi” ambayo shetani (kupitia nyoka) aliipandikiza ndani ya nafsi ya binadamu wa kwanza ambayo ndiyo itampa shetani kuendelea kujipatia wafuasi katika vizazi vya binadamu duniani. Na wenye roho hiyo ndio watakuwa mawakala wa kueneza uasi kwa binadamu duniani mpaka hapo “uzao wa mwanamke” utakapokuja kuziharibu kazi za Ibilisi na kuikomesha roho ya uasi.
UCHAMBUZI KUHUSU UZAO WA NYOKA
Msamiati wa uzao wa nyoka unajitokeza kwenye Agano jipya katika Injili ya Yohana Mbatizaji pale alipowaona makutano wakimwendea ili awabatize kama tunavyosoma hapa:
“Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.” (Lk.3:7-8)
Hapa tunasoma msamiati wa “enyi wazao wa nyoka”! Maneno haya haya tunakuta yanarudiwa kusemwa na Yesu Kristo mwenyewe na hasa akiwa amewalenga jamii ya mafarisayo waliokuwa wakimwandama kwa nia ya kutaka kumwangamiza: “Enyi wazao wa nyoka, mawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake..” (MT.12:34) Mahali pengine Yesu anawasema kwa ukali akiwakemea: “Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?” (Mt.23:33)
Kwa muktadha wa nukuu za maneno ya Yesu, walengwa wakuu wa msamiati wa “wazao wa nyoka” ni viongozi wa dini ya kiyahudi na maherodi ambao walikuwa wamekengeuka kiimani wakiongoza watu kwa udanganyifu. Kama viongozi waliokuwa wametishiwa na umaarufu wa Yesu Kristo walijawa na roho ya wivu na uchungu kiasi cha kuamua kutafuta kila mbinu wamwangamize. Na ukweli wa mambo ndivyo ulivyokuwa kwamba ni viongozi wa dini ndio walioongoza njama za kusulubishwa mpaka kuuawa kwa Yesu Kristo.
Kwa hiyo, uzao wa nyoka ni roho itendayo kazi katika wana wa kuasi mpango wa wokovu wa Mungu ulioletwa na Yesu Kristo duniani. Ni Kama Paulo alivyoandika akisema: “ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi.” (Efe.2:2)
Uzao wa nyoka ni roho ya kuasi ambayo imejizatiti katika kupinga mpango wa Mungu wa wokovu kupitia Yesu Kristo ili watu wasipate kuokolewa. Ndiyo maana waliopagawa na roho hii wanaitwa “wana wa kuasi” kutokana na ile roho inayowasukuma kuchochea hali ya uasi dhidi ya Injili ya Kristo. Kwa kifupi hawa ni viongozi walioteuliwa na Ibilisi kuendesha mkakati wake wa kuongoza uasi dhidi ya maadili ya kiimani kwa mujibu wa Injili ya Kristo.
UCHAMBUZI KUHUSU UZAO WA MWANAMKE
Kama tulivyokwisha kusoma hapo mwanzo ya kwamba, msamiati wa “uzao wa mwanamke” ulitamkwa na Mungu mwenyewe ukiwa ni unabii kuhusu ujio wa Yesu Kristo ambaye ndiye binadamu pekee mwenye sifa ya kuitwa “uzao wa mwanamke.”
Nabii Isaya ndiye aliyefunuliwa na kuandika kiunabii kuhusu huyu “uzao wa mwanamke” atakavyozaliwa: "Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli." (ISA. 7:14)
Hapa Isaya alipokea mafunuo kuhusu msichana “bikira” ambaye atabeba mimba na kuzaa mtoto mwanamume na kuitwa Imanueli. Miaka mingi baadaye unabii huu ukaja kutimia kwa bikira Mariamu kama Injili ya Mathayo inavyosimulia:
"Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao." (MT.1:18-21)
Kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma tunajifunza ya kwamba, uzao wa mwanamke ni Yesu Kristo ambaye hapo mwanzo alikuwa akiitwa Neno, na aliyekuwa kwa Mungu, na ambaye vitu vyote viliumbwa na yeye, na alikuwa Mungu, (YH.1:1-3) Kisha tunasoma ya kwamba alifanyika mwili akawa binadamu kamili duniani (YH.1: 14)
Baada ya Yesu aliyekuwa akiitwa Neno kufanyika mwili ndipo alianza kujitambulisha kwa jina la “Mwana wa Adamu”. Jina la Mwana wa Adamu limetumika katika Agano Jipya mara 97 na zote zikiwa zinamlenga Yesu mwenyewe. “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.” (YH.3:13)
Kwa habari ya uzao wa nyoka tulijifunza ya kuwa ni ““roho ya kuasi” ambayo shetani (kupitia nyoka) aliipandikiza ndani ya nafsi ya binadamu wa kwanza ambayo ndiyo itampa shetani kuendelea kujipatia wafuasi katika vizazi vya binnadamu duniani. Na wenye roho hiyo ndio watakuwa mawakala wa kueneza uasi kwa binadamu duniani” Aidha “uzao wa mwanamke” tulijifunza ya kuwa ni: ni unabii Mungu kuhusu ujio wa Yesu Kristo ambaye ndiye binnadamu pekee mwenye sifa ya kuitwa “uzao wa mwanamke.” Na ishara kuu ni kutimia kwa unabii wa bikira Mariamu aliyetunga mimba na kumzaa Yesu kama ilivyokuwa imetabiriwa na nabii Isaya.
Mwisho tulihitimisha sehemu ya kwanza kwa ahadi kwamba leo tutachambua vipengele vya aina mbili za “wana wa uzao wa nyoka” ambao wanajulikana kuwa ni “watoto wa Ibilisi” na “wana wa Mungu” ambao huzaliwa kiroho kupitia “uzao wa mwanamke” ambaye ni “Yesu Kristo” Mwana wa Adamu”.
UZAO WA NYOKA WA KIZAZI CHA WATOTO WA IBILISI
"Watoto wa Ibilisi" ni msamiati wa kibiblia ambao unawalenga binadamu kamili lakini wenye ushirika na Ibilisi kiroho! Haina maana kwamba Ibilisi naye ana uwezo wa kuzaa binadamu wa kimwili! Katika mada hii napenda kwanza tumchabue Ibilisi ni nani kabla ya kuwachambua "watoto wake"!
Yesu Kristo amemtaja Ibilisi na Shetani kwa nyakati tofauti katika Injili. Kila jina ambalo Yesu alilitumia linawakilisha tabia na kazi zake kamili!
Jina la kwanza la Ibilisi ni Shetani! Jina hili limetajwa mara 53 katika Biblia. Kwa lugha ya kiebrania ni satan na kwa kiyunani ni satana. Tafsiri ya jina hili maana yake ni adui, mpingaji, mpinzani, mshindani, mkinzani. Tabia na kazi yake ni kumpinga Mungu, wenye kumwamini Mungu, pamoja na kuwa kinyume na mambo yote yalivyo mema na haki.
Ibilisi! Kwa kiyunani ni Diabolos likimaanisha mshtaki (accuser) na mdhalilishaji (slanderer)! Kwa jina hili, Ibilisi huonyesha tabia na kazi zake ambazo ni kutengeneza tuhuma za kashfa za uongo kwa lengo la kuharibu heshima na hadhi ya mtu, kusingizia na kuchonganisha ili kuharibu mahusiano kati ya watu na Mungu na kati ya Mungu na watu
Mbali na majina haya mawili maarufu ya Ibilisi na Shetani; pia anayo majina mengine yanayo utambulisha ufalme wake ambao ni “falme na mamlaka, wakuu wa giza hili na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Efe 6:12) Katika ufalme wake anaitwa "mkuu wa ulimwengu huu"(Yh 12:31); mungu wa dunia hii (2 Kor.4:4); na mfalme wa uweza wa anga (Efe.2:2)
JINSI IBILISI ANAVYOZALISHA WATOTO
Yesu Kristo ndiye wa kwanza kumtaja Ibilisi kuwa na "watoto" pale alipokuwa akijibishana na jamii ya wayahudi waliokuwa wanapinga huduma zake za Injili: "Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda." (YN. 8:44)
Haya tukirejea kwenye maana iliyobeba jina "Ibilisi" ambayo ni "mshtaki na mdhalilishaji" utaona tabia hizi ndizo zilikuwa zimewajaa mafarisayo, masadukayo na waandishi!
Kazi yao ilikuwa ni kumchimba na kumtega Yesu wakitafuta namna ya kumvunjia heshima na hadhi yake mbele za watu ili kumharibia huduma yake; na hayo yote ni kwa sababu tu alikuwa anatishia maslahi yao binafsi na wao walighubikwa na hofu ya kupoteza umaarufu wao kwa wafuasi wao! Kwa tabia hizi, Yesu aliwaita "watoto wa Ibilisi"!
Ushahidi mwingine wa Yesu akitaja "watoto wa Ibilisi" ni pale aliposimulia mfano wa "mbegu njema" na magugu"! Wakati anatoa tafsiri ya mfano huo Yesu aliweka bayana kuhusu "konde" akisema ni "ulimwengu", na "mbegu njema" ni "wana wa ufalme" na "magugu" akasema ni "wana wa yule mwovu"! (MT. 13:38) Hapa tena tunakutana na msamiati wa "wana wa yule mwovu" ambaye ni Ibilisi
Njia kuu ambayo Ibilisi huitumia kuzaa watoto wenye kuitwa kwa jina lake ni "dhambi"! Kupitia tabia na matendo ya dhambi ndio utambulisho kamili wa kuwa "watoto wa Ibilisi": "...atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi." (1 YOH. 3:8)
Tukumbuke pia tafsiri ya dhambi ni "uasi" na ndivyo maandiko yanasemavyo: "kila atendaye dhambi afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi" 1.Yh.3:4) Kwa hiyo Ibilisi anazalisha watoto wake kupitia dhambi ambayo ni "roho" itendayo kazi katika "wana wa kuasi" (Efe.2:2)
Katika kuhitimisha kipengele hiki, napenda kuongezea uzito kuhusu "kiashiri" kikubwa cha kuwatambua "watoto wa Ibilisi" ni tabia sugu ya "kutokuamini" injili ya wokovu wa Yesu Kristo! Ni wapinzani, wabishi, wakali na wasiopenda kusikia habari za wokovu!
Wanaweza kuwa wanasali kwenye majengo ya ibada na hata kufanya huduma za kidini lakini mioyoni mwao ni jamii ya wasioamini! Haya si maneno yangu binafsi bali Yesu mwenyewe aliwadhihirisha akisema: “Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani atakayemsaliti.” (Yh.6:64)
Na sababu kubwa ya kutokuamini kwa "watoto wa Ibilisi" ni kwa kuwa "..... mungu wa dunia hii amepofusha akili zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ua utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” (2 Kor.4:4)
Ndiyo maana kwa wale tunaoamini tumetahadharishwa kutokufungiwa nira pamoja na wasioamini: “msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari?.....” (2 Kor.6:14-18)
CHIMBUKO LA KIZAZI CHA WATOTO WA MUNGU
Kuna nadharia mbili kuhusu msamiati wa “watoto wa Mungu” au “wana wa Mungu”. Nadharia ya kwanza inahusu uzao wa kimwili unaotokana na Adamu mpaka wakati wa gharika ya Nuhu. Hapa pia kuna kambi mbili zinazotofautiana kuhusu “wana wa Mungu”. Kambi ya kwanza inatafsiri “wana wa Mungu” ni malaika walioamua kuoa binti za wanadamu (Mw.6:1) Kambi ya pili inasema “wana wa Mungu” ni watoto wa Sethi mtoto wa kiume wa tatu wa Adamu ambaye kuanzia kwake ndipo watu walipoanza kuliitia jina la BWANA (Mw.4:25-26) Huu ni mjadala mwingine wa baadaye.
Nadharia ya pili kuhusu “watoto wa Mungu” inapatikana katika Agano Jipya! na hii ndiyo mada hii inajikita kwayo. Kwa mujibu wa tafsiri ya maandiko ya Injili ya Yohana, tunapewa tafsiri kuhusu watoto wa Mungu ya kuwa ni “kizazi cha kiroho” ambacho ni Jamii ya waliompokea na kumwamini Yesu Kristo: “..Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya amtu, bali kwa Mungu.” (Yh.1:11-12)
Kwa mantiki hii, Kila mwenye kuzaliwa na Mungu, anapokea uwezo maalum kutoka kwa Yesu moja kwa moja ambao unamfanya mhusika kuumbiwa upya rohoni mwake hali ya tabia ya uungu (2 Pet.1:4) Na hii inatokana na kazi aliyoifaanya Yesu Kristo msalabani ambapo kwa damu yake kuna muujiza wa kuzaliwa upya kwa mbegu isiyoharibika ya Neno la Mungu (1 Pet.1:23)
WATOTO WA MUNGU HAWATENDI DHAMBI
Najua kichwa cha somo hapa juu kikali na kunaleta utata. Lakini ndio ukweli wa kibiblia. Maandiko ya Yohana yanaweka bayana ya kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi na wala hawezi kutenda dhambi: “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Kwa hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.” (1 Yh.3:9-10) Mahali pengine imeandikwa tena: “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” (1 Yh.5:18)
TOFAUTI KATI YA WATOTO WA MUNGU NA WATOTO WA IBILISI
Kwa jamii ya “Watoto wa Ibilisi” utambulisho wao ni kuishi katika “mfumo wa dhambi” kama mtindo wa maisha. Pili, Kutokuiamini na kuipokea Injili ya wokovu wa Yesu Kristo ili wafanyike viumbe vipya ndani ya Kristo. Kwa jamii ya “Watoto wa Mungu” utambulisho wao ni “maisha ya utakatifu” kwa tabia na mwenendo (1 Pet.1:15) wakiwa hai na nuru ya ulimwengu (Mt.5:14) na chumvi ya dunia.(MT.5:13)
INAENDELEA SEHEMU YA TATU
Ninajua kwenye makala hii yako maswali mengi yanapita vichwani hivi sasa. Katika sehemu inayofuata nitajitahidi kupunguza baadhi ya maswali, hususan suala zima la “mtoto wa Mungu” kutokutenda dhambi tena. Kama sehemu hii imekugusa nijulishe kwa ku-like na warushie marafiki zako pia.
No comments:
Post a Comment