Na Mwl Christopher Mwakasege |
Leo tujifunze mfano wa 4 na mfano wa 5, juu ya jinsi Roho Mtakatifu anavyomuongoza mtu, kwa kutumia moto wa Mungu.
Mfano huu wa 4 unahusu “moto wa Mungu unapowaka ndani ya moyo wa mtu ukiwa umebeba taarifa ya ghadhabu na maonyo ya Mungu”
Tunasoma katika Isaya 66:15 ya kuwa: “Maana Bwana atakuja na moto…ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto”.
“Bwana atakuja na moto” ina maana ya Mungu kujifunua kwa njia ya – au kwa ishara ya “moto”. Na katika kujifunua huko, ndani ya moto huo – kuna ujumbe au taarifa ya “malipo ya ghadhabu yake”, na “maonyo yake”!
Kwa tafsiri iliyo rahisi utaona ya kwamba, “moto” wa jinsi hii, unapowaka moyoni mwako, ni kwa ajili ya kukupa onyo ya kuwa, kuna jambo lililomkasirisha Mungu, na lina adhabu inayokuja kama malipo ya kosa hilo!
Na ili ujumbe wa moto huu wa Mungu – unaokuja kwa jinsi hii – yaani uliobeba ghadhabu yake na maonyo yake – uweze kueleweka – huwa hauji peke yake!
Moto wa jinsi hii utawekwa na kudhihirishwa ndani ya moyo wa mtu na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ataambatanisha moto huu pamoja na “hofu ya Mungu”na “huzuni ya Mungu” na/au maombolezo, au/na kukunyima amani ya Kristo moyoni, na/au kukukosesha raha nafsini.
Hofu ya Mungu inapoambatana na moto wa Mungu moyoni mwa mtu – ni ujumbe toka kwa Roho Mtakatifu ya kuwa, moyo wa mtu huyo, usije ukadharau onyo hilo la ujio wa ghadhabu ya Mungu!
Na unapoona hofu ya Mungu ikiwa imeambatana na moto wa Mungu, unaona pia vimeambatana na au huzuni ya Mungu, au hali ya kuomboleza moyoni, au hali ya kukosa amani, au hali ya kukosa raha – ujue ni Roho Mtakatifu anakujulisha ya kuwa, pamoja na kwamba ghadhabu ya Mungu inakuja, LAKINI inaweza ikaepushwa kwa njia ya mtu kukubali maonyo na kutubu!
Hili tunalipata tunaposoma kitabu cha 2 Wakorintho 7:10 ya kwamba: “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto…”
Hivi ndivyo pendo la Mungu linavyofanya kazi, Mungu anapoghadhabika kwa sababu ya kosa la mtu! Roho Mtakatifu anampa mtu huyo taarifa ya ghadhabu hiyo – lakini pia na onyo – ambalo akilitii na kutubu – ghadhabu ya Mungu inafutwa na kuondolewa!
Fahamu jambo hili ya kuwa, Roho Mtakatifu anaweza kumuongoza mtu kwa jinsi hii:
(i) Kwa ajili ya mtu huyo mwenyewe;
(ii) au kwa ajili ya mtu mwingine ili apewe hiyo taarifa na kuombewa;
(iii) au kwa ajili ya eneo – kama mji, au kijiji, au kitongoji, au nchi, ili liombewe.
Nakuombea ili Mungu azidi kukupa ufahamu juu ya jambo hili, ili ijapo litatokea kwako, uweze kujua la kufanya.
Mfano huu wa 5 unahusu “moto wa Mungu unapowaka ndani ya moyo wa mtu, wakati mtu huyo anapokuwa katika mazingira yanayompa hasira, au yanampa kukata tamaa. Na kwa ajili hiyo Roho Mtakatifu anaweka hiyo “ishara” ya “moto wa Mungu” ndani ya moyo wa mtu huyo, ili kumwonya ajizuie kusema maneno – yatakayofanya hali yake ikawa mbaya zaidi!
Jaribu kubwa kwa mtu yeyote anayepitia kwenye mazingira magumu, au mazingira yaliyo kinyume na matarajio yake, ni kule kutaka kusema “maneno” yaliyojaa hasira, au yaliyojaa kukata tamaa!
Biblia inatueleza ya kuwa, Mungu aliwaongoza wana wa Israeli katika safari yao ya kutoka Misri na kwenda Kaanani, kwa “wingu” wakati wa mchana, na kwa “moto” wakati wa usiku (Hesabu 14:14).
“Wingu” wakati wa mchana na “moto” wakati wa usiku, vilikuwa ni ishara ya uwepo wa uongozi wa Roho Mtakatifu kwa ajili yao – wakati wote –yaani mchana na usiku. Ishara zote hizi mbili zilikuwa zinaonekana kwa macho wa mwili … kwa sababu agano lao na Mungu lilifungwa kwa ishara ya tohara ya mwili (Mwanzo 17:11-13).
Wakati huu wa kipindi cha agano jipya, ishara ya kuwa ni haki yako kuongozwa na Roho Mtakatifu-wakati wote-yaani mchana na usiku-ni mtu “kutahiriwa” moyo wake (Warumi 2:29).
Ingawa Mungu bado anaweza kutumia “wingu” na “moto” kuongoza watu wake akitaka; lakini kwenye kipindi hiki cha agano jipya, “mara nyingi” na kwa “sehemu kubwa”, anamuongoza mtu toka “ndani ya moyo wake”, kwa kumtumia Roho Mtakatifu aliyeingia ndani yake siku ile alipookoka!
Mazingira ya safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kwenda Kaanani hayakuwa mepesi. Mara nyingi walikutana na mazingira magumu na ya kukatisha tamaa – kwa jinsi ya kibinadamu! Na wakajikuta wanasema “maneno” ambayo yalionyesha ya kuwa “wamesahau” ukuu wa Mungu aliyekuwa pamoja nao wakati wote katika safari yao!
Ingawa Mungu alikuwa mvumilivu sana kwao, walipokuwa wanasema maneno magumu nay a kukata tama ….. wakiwa katika uwepo wake, na chini ya uongozi wake. Lakini hakuwa “mvumilivu” hivyo kwa wakati wote! Wakati mwingine aliwakasirikia sana aliposikia maneno waliyoyasema kiasi cha kuwaacha waingie katika shida zaidi!
Je, unakumbuka wana wa Israeli walisema nini, walipoletewa “habari mbaya” na wale wapelelezi kumi waliotumwa ili kuipeleleza nchi ya Kaanani?
Biblia inasema “wote wakamnung’unikia Musa na Haruni, …… wakawaambia, ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhari turudi Misri?” (Hesabu 14:2,3).
Maneno hayo hayakumfurahisha Mungu alipoyasikia! Kumbuka: Mungu alikuwa anajua ya kuwa “hali” iliyowafanya “wanung’unike”, na kukata tamaa ya kuendelea na safari yao na Bwana – ilikuwa “halisi”; na mazingira yalikuwa “halisi” pia!
Lakini “maneno” waliyoyasema katika “mazingira” yale, yalipeleka ujumbe uliokuwa mbaya masikioni mwa Mungu wao! “Bwana akamwuliza Musa, je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizi zote kati yao” (Hesabu 14:11)
Mungu akaendelea kusema hivi: “Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu unung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko….waninung’unikiao. Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi nilivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi..” (Hesabu 14:27,28). Na kwa sababu hii ya kuonyesha kutokuamini kwao kwa njia ya “maneno” waliyoyasema, walifia jangwani!
Ukiifuatilia vizuri habari hii, utaona ya kuwa katikati ya manung’uniko yale, na hasira walioonyesha juu ya Yoshua, na Kalebu, na Musa, na Haruni, “utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema la kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote” (Hesabu 14:10)
Wakati wa kipindi hiki cha agano jipya, mara nyingi “utukufu wa Bwana” utaonekana kwa ishara ya “moto” moyoni mwa mtu, KABLA hajasema “maneno” yatakayosababisha akwame zaidi!
Tunaposoma Yakobo 3:5, 6,9,10 tunaona ya kuwa: “ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Na ulimi ni moto …. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana . Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo”.
Ni dhahiri kwamba: kwa kuwa Mungu hataki uwashe “moto” kwa kinywa chako, utakaoleta shida kwako, na kwa wale wanaokuzunguka; anakuwekea ishara ya “moto” wake moyoni mwako unapopitia hali ngumu, ili kukupa “onyo” uchunge, na uzuie kinywa chako, na ulimi wako – usije ukasema maneno yatakayowasha “moto” utakaosababisha ukwame zaidi!
Mazingira ya namna hii yanapotokea kwako – utaona biblia inashauri yafuatayo:
(i) Omba Mungu awe anakuwekea “mlinzi” au “ulinzi” kwenye kinywa chako, ili usiwe unasema “maneno” yasiyofaa masikioni mwa Mungu, hata kama unapita katika mazingira magumu (Zaburi 39:1-3; Zaburi 14:1:3);
(ii) Jitahidi kukaa kimya bila kujibu au kujibizana – maana biblia inasema: “Laiti mngenyamaza kabisa! Hilo lingekuwa hekima kwenu” (Ayubu 13:5);
(iii) Tafakari na kuombea ahadi ya Mungu iliyopo katika neno lake, inayozungumzia juu ya jibu la Mungu katika kutatua tatizo hilo;
(iv) Ikiwa huna neno la namna hiyo, basi tafakari shuhuda za Mungu zilizomo katika biblia, na ulizozisikia katika maisha ya watu, zinazoonyesha ukuu, na uwezo, na utayari, wa Mungu katika kutatua matatizo kama uliyonayo;
(v) Usimdharau au kumkosea Mungu kwa kinywa chako! Ikiwa unajua umemkosea basi, tubu juu ya hilo! Ayubu alipokuwa anapitia hali ngumu ya maisha – biblia inasema: “katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake” (Ayubu 2:10).
(vi) Kila upatapo nafasi – na hata kama “akili” zako “ zinakubishia” endelea kukiri, na kushikilia ahadi za Mungu na uaminifu wa Mungu ….. naye atafanya (Warumi 4:20,21), na kumbuka rehema zake ni mpya kila asubuhi, ili tusiangamie (Maombolezo 3:22,23).
No comments:
Post a Comment