BWANA YESU asifiwe ndugu zangu.Karibu tujifunze.
Ndugu Zangu Huu Ni Wakati Wa Mwisho.
Wakati Kibiblia Unaweza Kumaanisha Miaka Kadhaa Ambayo MUNGU Ndie Ajuaye. Nyakati Moja Inaweza Hata Kuwa Na Zaidi Ya Miaka 1000.
2 Timotheo 3:1-7, Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda MUNGU; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi; wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.
Siku moja kama miezi miwili iliyopita nilikuwa kwenye gari la abiria maarufu kama costa nikitoka Kawe kwenda Ubungo, njiani kabla ya kufika Mwenge kuna dada mmoja alipanda gari na kukaa siti jirani na mimi, Dada yule alikuwa anasoma Gazeti ambalo nilipoliangalia nililiona kama jipya kwangu lakini la kidini, gazeti lile lilikuwa na vichwa vya habari vizuri sana na hakika ni gazeti linalovutia, nilitamani kulinunua gazeti hilo jipya la kikristo ambalo hakika halina udaku bali mambo mengi ya Biblia, nilimuomba dada yule aniambie linauzwa wapi. Nilipomwambia tu hivyo akanipa na kusema nichukue tu maana yeye anayo mawili ya toleo moja, muda kidogo yule dada akashuka kabla hata ya Mlimani city, Nilimshukuru kwa tendo lake jema la kunipa gazeti. Sikusoma kwa muda huo bali nilikusudia kusoma nikifika ubungo, ni kweli baadae nilianza kusoma na ndipo nilipojisemea kwamba ''Mwisho wa dunia umefika''. Gazeti hilo lilikuwa na kichwa cha habari kimojawapo kiitwacho ''KRISTO ANATAWALA NA KANISA'', Nilipenda kichwa cha habari hicho lakini nilipofungua ndani kuhusu ujumbe wa kichwa hicho cha habari nilikutana na kasheshe ambalo sijawahi kulisikia kabla. Yule Kristo anayetajwa sio BWANA YESU tunayemfahamu mimi na wewe bali ni mwanadamu mmoja ambaye kwa sasa ni marehemu na alikuwa kiongozi wa dhehebu moja la kikristo. huyo ndio anaitwa Kristo na licha ya kufariki bado waumini wake wanajua kwamba bado anatawala. Ufafanuzi wa taarifa hiyo ya kishetani gazetini ni kwamba BWANA YESU ni KRISTO wa kwanza lakini kizazi Hiki cha sasa eti MUNGU ameletwa kristo wa pili ambaye ni mwafrika wa Tanzania. Niliumia sana na kuwaza mengi sana na binafsi hadi leo naamini kwamba viongozi wa dhehebu hilo ni mawakala wa shetani na wapo kwa ajili ya kuhakikisha waumini wao hawaendi mbinguni. Waumini wa dhehebu hilo mimi siamini kama huwa wanasoma Biblia bali huwa wanasomewa tu. Nilichojifunza ni kwamba dhehebu hilo halina mpango wa waumini wake kwenda mbinguni. hili dhehebu ni hatari kama wachawi walivyo hatari, Hakika ni siku za mwisho.
Tunajua Kwamba Hizi Ni Siku Za Mwisho Kwa Sababu Ya Dalili Zilizoko Kwenye Biblia. Kama Wewe Unavyoweza Kujua Dalili Za Mvua Baada Ya Kuona Mawingu Ndivyo Hivyo Mwisho Umekaribia baada ya kila dalili kuonekana.
(1 Yohana 2:18-23, Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli. Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa YESU ni KRISTO? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye BABA na MWANA. Kila amkanaye MWANA, hanaye BABA; amkiriye MWANA anaye BABA pia. ).
Dalili za siku za mwisho ni nyingi, baadhi ni hizi:
1. Wapingakristo watatokea:hawa ni dini au watu binafsi ambao wanakataa ukombozi kupitia YESU KRISTO.
2. Watu kuliacha fundisho la KRISTO.
-Waongo ni wale wanaomkataa YESU na jambo la kukumbuka ni kwamba anayemkataa YESU huyo anamkataa MUNGU, Hakuna mtu aliye upande wa MUNGU kama amemkataa KRISTO katika maisha yake.
Hakika Ni Siku Za Mwisho.
3. Makristo Wa Uongo Wameshakuja(Mathayo 24:5,Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. ).
-Wengi hata sasa wameshakuja waongo na kuleta dini zao na wao kusimama kama nembo(icon) ya dini hizo, hawa hujifanya wakombozi wa watu na kwa hali hiyo hujifanya KRISTO.
-Wengi wanahubiri kama wanamhubiri KRISTO lakini ndani yao wana ajenda za kuzimu za kuwapotosha watu, hawawezi kukemea dhambi wala kufundisha toba.
4. Manabii Wa Uongo Wapo Na Hawakawii Kukwambia Kwamba YESU Atarudi Akiwa Shehe(Mathayo 24:24-27, Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. )
-Ndugu zangu, kuna watu hukimbilia miujiza, ndugu zangu sio kila wafanya miujiza ni watumishi wa MUNGU aliye hai, hata shetani naye ana watumishi wake ambao anawatumia.
-Mtu akileta fundisho tofauti na fundisho la KRISTO huyo ni nabii wa uongo.
-Wanaotangaza tarehe za kuja kwa YESU hao ndio hata hawajui walifanyalo.
Ndugu zangu mwisho umekaribia ila hakuna ajuaye siku wala saa, sisi tulichopewa kujua ni dalili tu na hakika dalili huonyesha kwamba mwisho umekaribia..
1 Petro 4:7 '' Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala. ''
5. Nyakati Za Mwisho Watu Watapenda Pesa Kuliko MUNGU Tena Wasaliti (2 Timotheo 3:1-7)
6. Nyakati Za Mwisho Watu Watasikiliza Mafundisho Ya Mashetani
7. Watajitenga Na Imani
8. Na Watazuia Watu Kuoa
9. Na Watakataza Watu Kula Baadhi Ya Vyakula
1 Timotheo 4:1-4 ''Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha MUNGU ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; ''.
10. Siku Za Mwisho Watu Watajaa Dhihaka 2 Petro 3:3-4 '' Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake(YESU)? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. ''
11. Watu wengi watakua Hawana ROHO MTAKATIFU(Yuda 1:18-21, ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu. Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na ROHO. Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya BWANA wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. ).
Ndugu Zangu Wanamume Kwa Wanawake YESU KRISTO Anatuita Kwenye Ufalme Wake. Amua Vyema Leo Kwa KUOKOKA.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.
No comments:
Post a Comment