Hili ni vazi ambalo huvaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu na Patriaki wa Yerusalem tu. Ieleweke wazi kuwa siyo kila Askofu Mkuu huvaa Pallium. La hasha! Huvaliwa tu na Maaskofu Wakuu ambao ni Maaskofu-Jimbo (yaani wana majimbo wanayoyaongoza).
Hata hivyo, huvaliwa tu na Askofu Mkuu awapo ndani ya majimbo yanayounda Jimbo Kuu lake. Mfano Jimbo Kuu la Mwanza linaundwa na majimbo ya Mwanza, Musoma, Shinyanga, Bunda, Geita, Kayanga, Bukoba na Rulenge-Ngara. Hivyo Askofu Mkuu wa Mwanza anaweza kuvaa Pallium awapo kwenye mojawapo ya majimbo hayo. Akienda Jimbo la Tanga, kwa mfano, hawezi kuvaa Pallium kwa sababu ni nje ya metropolitan yake (nje ya mipaka ya Jimbo Kuu la Mwanza).
Pallium hutokana na sufu (manyoya ya kondoo) yaliyokatwa kutoka kwa kondoo wakati wa sherehe ya Mt. Anyesi ambayo huadhimishwa Januari 21 kila mwaka. Jina Anyesi (au Agnes) limetokana na neno la Kilatin “Agnus” lenye maana ya “Mwanakondoo”. Kwa nini hutengenezwa kutokana na sufu ya kondoo? Kwenye Agano Jipya Kristo anatambulishwa kama “Mwanakondoo wa Mungu” (rejea Yn. 1:29, 36). Kama ambavyo kondoo wanatoa sufu kwa ajili ya kutengeneza Pallium.
hivyo hivyo Kristo aliye “mwanakondoo wa Mungu” anajitoa sadaka kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Kadhalika, kitendo cha kuvaa shingoni Pallium iliyotengenezwa kutokana na sufu ya kondoo kinaonesha kuwa Askofu ni Mchungaji Mwema kwani amewabeba kondoo zake (waamini) mabegani. Pallium inapovaliwa shingoni mwa Askofu inamaanisha pia “nira ya Kristo” kwani Kristo alisema “Jitieni nira yangu… Kwa maana nira yangu ni laini…” (Mt. 11:29, 30). Pallium zikishatengenezwa huweka chini ya altare ya Basilica la Mt. Petro karibu kabisa na kaburi la Mtume Petro. Kila tarehe 29 June ambayo ni Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Maaskofu Wakuu wapya walioteuliwa mwaka huo huenda Roma na kupatiwa Pallium hizo kama zawadi maalumu kutoka kwa Baba Mtakatifu.
Kwa nini Pallium huwekwa karibu na kaburi la Mtume Petro? Na kwa nini Papa pekee ndiye huwapatia Pallium Maaskofu Wakuu? Hii ni kuonesha kuwa Maaskofu Wakuu wanapaswa kuwa na ushirika wa kipekee kabisa na Baba Mtakatifu ambaye ni halifa wa Mtume Petro. Wanapaswa kuonesha muungano na utii kwa Baba Mtakatifu ambaye ni halifa wa Mtume Petro. Pallium ni nyeupe ili kuonesha kuwa Askofu husika anapaswa kuwa na usafi wa maisha (innocence of life).
Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu la Mwanza
(ARTICLE FROM TEC FACEBOOK, 2020)
No comments:
Post a Comment