Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Annegret Kramp-Karrenbauer amesema Ujerumani haijapokea taarifa rasmi kutoka Marekani kuhusu mpango wa nchi hiyo kuwaondoa baadhi ya wanajeshi wake Ujerumani.
Akizungumza leo na waandishi habari, Kramp-Karrenbauer amesema hawezi kuzungumzia taarifa za kwenye vyombo vya habari bila ya kuwepo uthibitisho.
Kiongozi huyo wa chama cha Christian Democratic Union, CDU amesema ukweli ni kwamba uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Ujerumani unatumika kuimarisha usalama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na washirika wengine wa NATO pamoja na Marekani yenyewe.
Amesema huo ndiyo msingi ambao unaleta ushirikiano wa pamoja kati ya nchi hizo. Naye msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amesema Ujerumani itatoa tamko mara itakapopewa taarifa na Marekani.
Siku ya Ijumaa, afisa wa ngazi ya juu wa Marekani, alisema kuwa Rais Donald Trump aliliamuru jeshi la Marekani kuwaondoa askari wake 9,500 kutoka Ujerumani.
(MUUNGWANA BLOG, June 2020)