Lissu Atangaza Nia ya Kuwania Urais 2020

Share it Please




Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tundu Lissu leo amezungumza kwa Mubashara kupitia ukurasa wake wa Facebook akiwa ughaibuni na kutangaza nia ya kugombea Urais nchini Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa October 2020.

Lissu amechukua hatua hiyo siku kadhaa tangu John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, kuwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, kuwasilisha taarifa zao katika ofisi yake, kuanzia tarehe 3 hadi 15 Juni 2020.

Lissu amesema, endapo atafanikiwa kuwa Rais, ataboresha uchumi wa nchi, mahusiano na jumuiya za kimataifa na nchi marafiki, utawala bora, misingi ya haki za binadamu, demokrasia na mfumo wa vyama vingi.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu, utaamua kama Chama cha Mapinduzi (CCM), kitapata fursa ya miaka mitano mingine ya kuendelea kuharibu uchumi wa nchi na kufukarisha wananchi, au mwanzo mpya kwa Tanzania, kujiimarisha kiuchumi.

Lissu amesema, akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha mihimili ya nchi, ikiwemo Bunge na Mahakama, inakuwa huru na kujitegemea kwenye maamuzi yake.

Amesema katika uongozi wake kama atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, atavitumia vyombo vya ulinzi na usalama kulinda haki za binadamu, na si katika kukandamiza wapinzani wake, vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Amesisitiza kuwa endapo atafanikiwa kuwa Rais, Serikali yake itaendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala bora na sheria, inayoendana na Katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa, ambayo Tanzania iliikubali.

Lissu amesema, akifanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, ataponya majeraha ya wananchi pamoja na kurejesha umoja wa kitaifa, huku akisisitiza kwamba hatalipa kisasi kwa maadui zake.


(GLOBAL PUBLISHER JUNE 8 2020)