Maharage
ni chakula ambacho watu wengi hukichukulia kama chakula cha hadhi ya
chini kisichokuwa na manufaa kiafya. Watu wengi huchukulia vyakula kama
vile nyama na samaki kuwa ni vya kitajiri wakati maharage yakichukuliwa
kuwa ni chakula cha kimaskini.
Huu ni upotoshaji, kwani maharage yana faida nyingi sana mwilini ambazo watu wasiokula maharage wanazikosa.
Kwa kuwa lengo letu ni kukupa maarifa, basi karibu ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu faida 19 za kula maharage.
1. Hupunguza lehemu (cholesterol)
Moja
kati ya vyakula vinavyopunguza lehemu mwilini ni maharage. Nyuzinyuzi
zinazopatikana kwenye maharage hujishikiza na lehemu ziwapo tumboni na
kuzuia lehemu zaidi kufyonzwa mwilini.
2. Huzuia saratani
Maharage
ni chakula chenye madini ya manganese pamoja na vitamini K ambavyo
vyote kwa pamoja huzuia kuharibika kwa seli kunakosababisha saratani.
3. Huboresha afya ya ubongo
Kemikali ya thiamine pamoja na vitamini K zinazopatikana kwenye maharage husaidia katika kuboresha afya ya ubongo.
4. Hutawala kiwango cha sukari mwilini
Maharage
yana nyuzi nyuzi ambazo hupunguza kiwango cha metaboli cha wanga
(carbohydrates) mwilini. Kwa kufanya hivi huwezesha kutawala kuongezeka
kwa kiwango cha sukari hasa baada ya kula chakula.
Maharage pia yana protini ambayo husaidia kupunguza kiwango cha sukari mwilini.
5. Huongeza nguvu za mwili
Kuwepo kwa madini ya chuma pamoja na manganese kwenye maharage kunayafanya kuwa na nafasi kubwa katika kuongeza nguvu za mwili.
Madini haya ni muhimu sana katika kuuongezea na kuupa mwili nguvu.
6. Huimarisha mifupa
Madini
ya calcium pamoja na manganese ni muhimu sana kwa ajili ya afya ya
mifupa. Maharage ni chanzo kimojawapo kizuri cha madini haya.
7. Huboresha ngozi
Maharage
husaidia michakato ya metaboli ya asidi ya amino, gluconeogenesis,
neurotransmitter synthesis, histamine synthesis, asidi ya mafuta (fatty
acids), lipids and hemoglobin synthesis kwenda vizuri.
Ikumbukwe kuwa hivi vyote vina nafasi kubwa katika kuboresha afya ya ngozi.
8. Huboresha afya ya moyo
Aina nyingi za maharage zina vitamini B9 (folate au folic acid) ambayo ni muhimu kwa ajili ya afya ya misuli ya moyo.
9. Huboresha afya ya macho
Madini
ya zinc yanayopatikana kwenye maharage ni muhimu sana kwa ajili ya afya
ya macho. Hivyo ulaji wa maharage mara kwa mara utaboresha afya ya
macho yako.
10. Huboresha uwezo wa kumbukumbu
Kama
nilivyotangulia kusema kuwa maharage huboresha afya ya ubongo, uwezo wa
kumbukumbu huboreshwa pia kupitia ulaji wa maharage.
Vitamini B1 inayopatikana kwenye aina mbalimbali za maharage hukabili ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer’s na dementia).
11. Huondoa sumu mwilini
Vyakula
vingi vya viwandani huhifadhiwa kwa kutumia vihifadhi vyenye sulphites;
Sulphites inapozidi mwilini ni sumu. Hivyo basi kemikali ya molybdenum
inayopatikana kwenye maharage inasaidia kuondoa sumu ya sulphites
mwilini.
12. Hukabili shinikizo la damu
Kama
tulivyoeleza kwenye makala nyingine, potassium, magnesium pamaoja na
protini husaidia sana kukabili shinikizo la juu la damu. Maharage
hukabili shinikizo la damu kwa kuwa ni chanzo kizuri cha potassium,
magnesium pamoja na protini.
13. Hupunguza uzito
Vyakula
kama maharage vina nyuzinyuzi zinazokuwezesha usihisi njaa mapema,
hivyo kuepuka kula mara kwa mara na kusababisha kuongeza uzito wako.
Ikumbukwe pia maharage ni chakula ambacho kina kiwango kidogo cha mafuta (fat), hivyo hakisababishi uzito mkubwa wa mwili.
14. Husaidia kutibu tatizo la kutokupata choo
Kama
nilivyoeleza kwenye hoja zilizopita, maharage ni chakula chenye
nyuzinyuzi kwa wingi; ikumbukwe kuwa vyakula vyenye nyuzinyuzi ni tiba
bora ya tatizo la kutokupata choo.
15. Husafisha tumbo
Wakati baadhi ya watu wakiyachukulia maharage kama kitu kinachovuruga tumbo, maharage yana nafasi kubwa kwenye afya ya tumbo.
Utafiti
uliofanyika ulibaini kuwa kula maharage kwa kiasi cha kutosha
kutasafisha tumbo lako na kukukinga na maradhi ya saratani ya utumbo
(colon cancer).
16. Husaidia kukabili maradhi ya asthma
Utafiti
uliofanyika ulibaini kuwa kuna uhusiano kati ya upungufu wa madini ya
magnesium na kutokea kwa maradhi ya asthma. Kutokana na maharage kuwa na
kiwango kizuri cha madini ya magnesium, basi yanaweza kuwa na mchango
mkubwa katika kukabili maradhi haya.
17. Huboresha na kukomaza seli nyekundu za damu
Virutubisho vilivyoko kwenye maharage husaidia katika maendeleo na ukomavu wa seli nyekundu za damu.
18. Huzuia kuzeeka mapema
Kuzeeka
mapema? Ndiyo, kutokana na maharage kuwa na kemikali zinazozuia
kuchakaa kwa seli za mwili, yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika
kuzuia kuzeeka mapema.
19. Huboresha afya ya kucha na nywele
Biotin,
madini ya chuma pamoja na protini vinavyopatikana kwenye maharage vina
nafasi kubwa katika kukupa kucha imara pamoja na nywele zenye afya
njema.
Neno la mwisho
Je
bado huoni umuhimu wa maharage katika afya ya mwili wako. Anza kula
maharage uboreshe afya ya mwili wako sasa. Ikizingatiwa kuwa maharage ni
chakula kinachopatikana kwa bei rahisi tofauti na vyakula vingine kama
vile nyama na samaki, hivyo huna kisingizio chochote.
No comments:
Post a Comment